Moyo Wangu

Moyo wangu sio mpira, mateke kuupigapiga
Usinipakulie zako hasira, mie sio yako tiba wala kinga
Ilikushinda subira, ombi langu ukalipingapinga
Kwa nilivokutumainia, ukaonelea bora kutangatanga

Moyo wangu sio danganyadanganya, umechoka kuhanywahanywa
Huba langu aminifu, na wengine Sitaki kuchanganywachanganywa
Moyo wangu hupenda kikamilifu, hata ukinyanyaswanyanyaswa
Moyo wangu mzinga wa asali kuugundua, kuila nyuki watakusumbua

Moyo wangu ni harusi, moyo wangu ni matanga
Nkikuzawadi ni kama harusi, sipoutunza ni yako majanga
Moyo wangu una wake weusi, moyo wangu una wake mwanga
Moyo wangu thamani, katu siupeani kihubahuba tena asilani…

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started